Ukristo
kutoka neno la Kigiriki Χριστός, Khristos, ambalo
linatafsiri lile la Kiebrania , Māšîăḥ, linalomaanisha "Mpakwamafuta"
[1]) ni dini inayomwamini Mungu pekee[2] kama alivyofunuliwa kwa Waisraeli
katika Agano la Kale na hasa na Yesu Kristo, mwanzilishi wake, katika karne ya
1.
Dini hiyo, iliyotokana na ile ya Wayahudi, inalenga kuenea
kwa binadamu wote, na kwa sasa ni kuu kuliko zote duniani,[3][4][5] ikiwa na
wafuasi 2,400,000,000 (33% kati ya watu 7.274 bilioni)[6][7][8][9], ambao nusu
ni waamini waKanisa Katoliki na nusu ya pili wamegawanyika katika madhehebu
mengi sana.
Kitabu chake kitakatifu kinajulikana kama Biblia. Ndani yake
inategemea hasa Injili na vitabu vingine vya Agano Jipya.
Kati ya madhehebu ya Ukristo, karibu yote yanamkiri Yesu
kuwa kwa pamoja Mungu kweli na mtu kweli: katika umojana nafsi yake ya Kimungu
zinapatikana sasa hali hizo zote mbili.
Yote yanamkiri kuwa Mwokozi wa watu wote, na kuwa ndiye
atakayerudi mwishoni mwa dunia kwa hukumu ya wote, ingawa maelezo kuhusu jambo
hilo yanatofautiana.
Vilevile yote yanamchukua kama kielelezo cha utakatifu
ambacho kiwaongoze katika maadili yao maalumu, kuanziaunyenyekevu na upole hadi
upendo unaowaenea wote, bila kumbagua yeyote, hata adui.
Asili
Chimbuko la Ukristo ni kuwepo kwa mtu aliyezaliwa takriban
miaka 2000 iliyopita huko Mashariki ya Kati, katika kijiji cha Bethlehemu kilichopo
hadi hivi leo kwenye mipaka ya Palestina; alikuwa akiitwa Yesu wa Nazareti
(kijiji alikokulia) au mwana wa Yosefu mchonga samani; mama yake akifahamika
kwa jina la Bikira Maria.
Kwa kumuita pia Kristo, wafuasi wake walikiri kwamba ndiye
aliyetimiza utabiri wa manabii wa kale, kama unavyopatikana katika vitabu vya
Biblia ya Kiebrania na Deuterokanoni.
Masiya Yesu
Ukristo ni matokeo ya utume wa Yesu, uliopokewa na waliomwamini
kuwa ndiye Masiya, yaani mkombozi aliyetimiliza ahadi za Mungu kwa binadamu.
Katika kitabu cha Mwanzo tunasoma utabiri wa kuja kwake
ulianzia katika bustani ya Edeni pale Mungu alipomwambia nyoka, yaani shetani,
kuhusu mwanamke kwamba "uzao wake utakuponda kichwa" (Mwa 3:15).
Baadaye Abrahamu, babu wa taifa la Israeli, kwa imani na
utiifu wake kwa Mungu, aliahidiwa kwamba katika uzao wake mataifa yote yatabarikiwa.
Musa, mwanaharakati aliyewakomboa watu wa Israeli kutoka
utumwani Misri takribani miaka 1250 KK (kabla ya kuzaliwa kwa Yesu), ndiye
nabii wa kwanza kutabiri wazi kwa niaba ya Mungu ujio wa Masiya au Kristo (Kumb
18:15-22, hususan mstari 18: "Nitawainulia nabii kama wewe kutoka miongoni
mwa ndugu zenu; na nitatia neno langu kinywani mwake na atasema nao yote
niliyomwamuru."
Kuja kwake kulitimia katika Agano Jipya, ambalo ni ukamilifu
wa yote yaliyotabiriwa katika Agano la Kale. Kwani Musa alitumwa kuanzisha
Agano la Kale kama maandalizi ya Agano Jipya, akikabidhi mifumo mingi ya nje na
ndani kwa watawala na waamuzi waliomfuatia watakaoshikilia Agano la kusubiri
Masiya wakishirikiana na manabii na makuhani.
Yesu alizaliwa miaka kama 1800 baada ya Abrahamu. Vitabu vya
Injili vinaeleza matukio na mafundisho ya Yesu ambayo ndiyo mwongozo wa imani hiyo.
Maisha na kazi ya Yesu vimeibua mambo mengi katika historia. Ndiyo sababu
kalenda iliyoenea duniani huhesabu miaka kutoka ujio wake; huu ni mchango
mmojawapo wa Ukristo katika ustaarabu.
Mafundisho ya msingi ya Yesu
Hotuba ya Mlimani
kadiri ya Carl Heinrich Bloch.Hotuba ya Mlimani inachukuliwa
na Wakristo kuwa utimilifu wa Torati iliyotolewa na Musa katika Mlima Sinai.
Yesu alifanya ishara za kustaajabisha, au miujiza. Matokeo
ni kwamba, watu wengi wakamwamini.
Nikodemu, mshiriki mmojawapo wa baraza la Sanhedrini, ambalo
lilikuwa pia mahakama kuu ya Wayahudi, alivutiwa na kutaka kujua zaidi kuhusu
siri ya miujiza hiyo na ujumbe kutoka kwa Mungu; kwani yeye alihamasika kuona
ishara zile kutoka kwa Mungu.
Yesu akamjibu kwamba hakika mtu hawezi kuingia ufalme wa
Mungu asipozaliwa mara ya pili kwa maji na Roho Mtakatifu.
Pia akajieleza kuwa mpatanishi wa ulimwengu wa dhambi na
Mungu na kwamba kila anayemgeukia kwa imani hatapotea, bali atarithi uzima wa
milele: alisema mwenyewe ni mfano wa nyoka wa shaba aliyetengenezwa na Musa.
(Yoh 2:23-3:21; Hes 21:9).
Akiwa kando ya Ziwa la Galilaya, Yesu alikuta umati wa watu
umekusanyika. Basi akapanda mashuani na kuenda mbali kidogo naufuoni, akaanza
kuwafundisha kuhusu Ufalme wa mbinguni kupitia mfululizo wa mifano.
Mmojawapo ni huu ufuatao: "Ufalme wa mbinguni ni kama
punje ya haradali ambayo mtu anaipanda. Ingawa ni mbegu ndogo sana inakua na
kuwa mti wa mboga mkubwa kuliko yote. Inakuwa mti ambao ndege wanauendea,
wakipata makao katika matawi yake". (Math 13:1-52; Mk 4:1-34; Lk 8:4-18;
Zab 78:2; Isa 6:9,10).
Kanisa siku za mwanzo
Umoja wa waamini na Kristo ndio lengo la Ukristo.
Jumuia ya Wakristo inaitwa Kanisa, yaani
"mkusanyiko" kama lilivyotajwa na Yesu mwenyewe hasa katika Injili ya
Mathayo 16:18:
Wewe ndiwe Petro na juu ya mwamba huu, nitalijenga kanisa
langu. Wala milango ya kuzimu haitalishinda.
Yesu aliita wengine 11 pamoja na Petro kuunda kundi la
mitume wake. Idadi yao ilipangwa kwa kusudi la kudokeza kwamba ndiyo mwanzo
mpya wa taifa la Mungu, kama vile watoto 12 wa Yakobo Israeli walivyokuwa
mwanzo wa taifa lake la kale.
Yesu aliwapa hao Thenashara mamlaka ile aliyopewa na Mungu
Baba ili kuokoa watu.
Yesu na wanafunzi wake wa kwanza walikuwa Wayahudi. Yaani
walizaliwa katika uzazi wa Abrahamu wakiwa watoto wa Agano lililofanywa kati ya
Mungu na taifa lake la Israeli zamani za Musa.
Wakati wa Yesu Waisraeli hao waliitwa "Wayahudi".
Walio wengi waliishi nje ya nchi ya Israeli/Palestina, kutokana na vita vingi
vya zamani vilivyosababisha wakimbizi kuhamia nchi zenye usalama zaidi. Jumuiya
za Wayahudi zilipatikana katika miji yote mikubwa yaAfrika Kaskazini (hasa
Misri na Libia), Ulaya Kusini na Asia Magharibi mpaka Uajemi.
Kwa upande mmoja Wayahudi walitoka katika ukoo wa Ibrahimu,
hasa waliokaa Israeli/Palestina. Lakini watu wengine wenye asili ya mataifa
tofauti waliwahi kujiunga na imani ya Wayahudi na kuchukua hatua ya kuongoka na
kutahiriwa.
Katika mazingira yao Wayahudi walikuwa watu wa pekee
waliomshuhudia Mungu mmoja tu. Walikuwa tofauti na wengine kwani hawakushiriki
katika ibada ya miungu ya serikali, tena walitunza utaratibu wa sabato yaani
kutotenda kazi siku ya saba.
Mitume wa Yesu walizunguka awali hasa katika jumuiya za
Wayahudi kila mahali walipokwenda. Mwanzoni Kanisa lilionekana kama dhehebu la
Kiyahudi tu. Baada ya kupokea watu kutoka mataifa bila kuwatahiri hali
ilibadilika: Kanisa likawa taifa la Mungukutoka kwa Wayahudi na kwa Mataifa.
itaendlea....................................................
No comments:
Post a Comment